Sheria za Jukwaa, vifungu 12 vinavyolinda kila mtumiaji.

Hii ni hati kamili inayosimamia matumizi yote ya jukwaa la Siri za Chumbani, kuanzia ulinzi wa utambulisho wako, hadi wajibu wako kwa watumiaji wengine. Soma kila kifungu hapa chini, au pakua PDF rasmi.

ToleoJulai 2026
Vifungu12 Rasmi
Imesasishwa29 Julai 2026
LughaKiswahili

Siri za Chumbani ni jukwaa la anonymous confession linalowapa watu nafasi ya kushiriki siri, hisia, changamoto na matukio mbalimbali ya maisha yao bila kufichua utambulisho wao.

Sheria hizi zimewekwa ili kuhakikisha kuwa jukwaa hili linabaki kuwa sehemu salama, yenye heshima na inayolinda faragha ya kila mtumiaji. Lengo la sheria hizi si kuzuia uhuru wa mtu kueleza yaliyopo moyoni mwake, bali kuhakikisha kuwa uhuru huo unatumiwa kwa uwajibikaji na bila kuathiri usalama wa wengine. Kwa kutumia jukwaa la Siri za Chumbani, kila mtumiaji anakubaliana kuheshimu sheria na miongozo yote iliyowekwa hapa chini.

01

Hairuhusiwi Kushiriki Taarifa Binafsi

Mtumiaji wa Siri za Chumbani haruhusiwi kuweka taarifa binafsi ndani ya confession yake ambazo zinaweza kumtambua yeye au mtu mwingine.

Taarifa binafsi zinahusisha namba ya simu, barua pepe (Email), taarifa za malipo kama LIPA namba au control number, majina ya akaunti za mitandao ya kijamii kama Instagram, Facebook, Telegram, Twitter (X) au taarifa nyingine yoyote inayoweza kuvunja mfumo wa anonymous wa jukwaa hili.

Sheria hii imewekwa kwa sababu msingi mkuu wa Siri za Chumbani ni kulinda utambulisho wa watumiaji. Mtumiaji anatakiwa kushiriki ujumbe wake bila kuweka taarifa ambazo zinaweza kusababisha yeye au mtu mwingine kufahamika.

Hatua Zitakazochukuliwa

Confession yenye taarifa binafsi inaweza kuzuiwa na mfumo wetu wa ukaguzi na haitachapishwa kwenye majukwaa yetu. Katika baadhi ya mazingira, mtumiaji anaweza kuzuiwa kutumia huduma ya kutuma confession kwa muda maalum.

02

Hairuhusiwi Kuomba Msaada wa Kifedha

Siri za Chumbani si jukwaa la kuomba michango, fedha au msaada wa kifedha wa aina yoyote.

Hairuhusiwi kutuma confession yenye lengo la kuomba fedha kwa ajili ya ada, matibabu, chakula, biashara, matatizo binafsi au sababu nyingine yoyote ya kifedha.

Tunaelewa kuwa watu wengi wanapitia changamoto mbalimbali na tunaheshimu hali zao, lakini jukwaa hili limeanzishwa kwa lengo la kutoa nafasi ya watu kueleza siri, hisia na mambo mazito yaliyopo mioyoni mwao.

Hatua Zitakazochukuliwa

Ujumbe wowote unaoonekana kuwa ni ombi la msaada wa kifedha unaweza kuzuiwa moja kwa moja na mfumo wetu wa ukaguzi au timu ya usimamizi.

03

Hairuhusiwi Kutafuta Utambulisho wa Mtumaji wa Confession

Siri za Chumbani inalinda anonymity ya kila mtumiaji. Hairuhusiwi kujaribu kumtambua, kumtafuta au kuomba mawasiliano ya mtu aliyeshiriki confession kwenye jukwaa.

Watumiaji hawaruhusiwi kuomba namba ya simu, akaunti za mitandao ya kijamii au taarifa nyingine zinazoweza kumtambua mtumaji wa confession. Sheria hii inalinda usalama wa watu wanaochagua kufungua mioyo yao kupitia jukwaa hili bila hofu ya kufichuliwa.

Isipokuwa: Endapo confession imetumwa kupitia huduma maalum ya kutafuta mwenza kama Siri Couple Connect, utaratibu huo utasimamiwa tofauti kwa sababu mtumiaji ameonyesha wazi kuwa anatafuta mahusiano.
Hatua Zitakazochukuliwa

Maombi yoyote ya kuvunja anonymity ya mtumiaji yanaweza kuondolewa na mtumiaji anaweza kuzuiwa kutumia huduma kulingana na uzito wa kosa.

04

Hairuhusiwi Maudhui ya Kisiasa

Siri za Chumbani haliruhusu matumizi ya jukwaa kwa mijadala ya kisiasa, kampeni, propaganda au mashambulizi yanayohusiana na siasa.

Lengo la jukwaa ni kutoa nafasi kwa watu kushiriki uzoefu binafsi, hisia na siri zao bila kuleta migawanyiko ya kisiasa ndani ya jamii ya watumiaji.

Hatua Zitakazochukuliwa

Confession au ujumbe wenye maudhui ya kisiasa unaweza kuzuiwa na hautachapishwa.

05

Hairuhusiwi Ubaguzi na Chuki Dhidi ya Wengine

Siri za Chumbani halikubali ubaguzi wa aina yoyote.

Hairuhusiwi kutumia jukwaa hili kueneza ubaguzi wa rangi, kijinsia, kikabila, kidini, ulemavu au aina yoyote ya chuki dhidi ya kundi au mtu mwingine.

Siri za Chumbani inalenga kuwa sehemu ambayo watu wote wanaweza kushiriki bila kuhisi kutengwa, kushambuliwa au kudhalilishwa.

Hatua Zitakazochukuliwa

Maudhui yenye ubaguzi au chuki yataondolewa na mtumiaji anaweza kuzuiwa kutumia huduma za jukwaa.

06

Heshima Kwenye Maoni na Majadiliano

Siri za Chumbani inaruhusu watu kutoa maoni kuhusu confession mbalimbali, lakini maoni hayo lazima yawe ndani ya mipaka ya heshima.

Hairuhusiwi kutumia sehemu za maoni kuweka matusi, vitisho, lugha ya chuki, kashfa au kumshambulia mtu mwingine binafsi.

Kutoa maoni ni sehemu muhimu ya kujenga jamii, lakini lazima kufanyike kwa heshima na uelewa.

Hatua Zitakazochukuliwa

Mtumiaji anayekiuka sheria hii anaweza kuzuiwa kutoa maoni kwenye mitandao yetu ya kijamii au tovuti ya Mnyilinga Hub.

07

Hairuhusiwi Maudhui ya Kingono Yasiyoruhusiwa

Siri za Chumbani hairuhusu matumizi ya jukwaa hili kwa kushiriki maudhui ya kingono ambayo yanakiuka heshima, usalama au sheria za jamii. Hairuhusiwi kutuma confession yenye:

  • Maelezo ya kingono yaliyo wazi kwa lengo la kuchochea au kusambaza maudhui yasiyofaa.
  • Picha, video au viungo vya maudhui ya kingono.
  • Maudhui yanayohusisha kulazimisha, unyanyasaji wa kingono au vitendo vya kingono bila ridhaa.
  • Maudhui yoyote yanayoweza kuhatarisha usalama au utu wa mtu mwingine.

Siri za Chumbani inaruhusu watu kueleza changamoto zao binafsi kuhusu mahusiano na maisha ya kimapenzi, lakini maudhui hayo lazima yabaki ndani ya mipaka ya heshima na yasigeuke kuwa maudhui yasiyofaa.

Hatua Zitakazochukuliwa

Confession au ujumbe wenye maudhui ya kingono yasiyoruhusiwa utazuiwa na hautachapishwa kwenye majukwaa yetu. Ukiukwaji mkubwa unaweza kusababisha mtumiaji kuzuiwa kutumia huduma za Siri za Chumbani.

08

Hairuhusiwi Vitisho, Vurugu au Kuhamasisha Madhara

Siri za Chumbani hairuhusu ujumbe wowote unaotishia usalama wa mtu mwingine au kuhamasisha vitendo vya vurugu. Hairuhusiwi:

  • Kutishia kumdhuru mtu.
  • Kuhamasisha vurugu au kulipiza kisasi.
  • Kutoa maelekezo ya kufanya madhara kwa mtu mwingine.
  • Kusherehekea au kuunga mkono vitendo vya ukatili dhidi ya watu.

Tunaelewa kuwa baadhi ya watu wanaweza kushiriki hisia kali kutokana na maumivu au hasira, lakini jukwaa hili halipaswi kuwa sehemu ya kueneza vitisho au madhara.

Hatua Zitakazochukuliwa

Maudhui yenye vitisho au vurugu yataondolewa mara moja na mtumiaji anaweza kuzuiwa kutumia jukwaa.

09

Hairuhusiwi Kushiriki Taarifa za Watoto

Siri za Chumbani inalinda usalama na faragha ya watoto. Hairuhusiwi kushiriki taarifa zinazoweza kumtambua mtoto au kumuweka katika hatari. Hii inajumuisha:

  • Majina kamili ya watoto.
  • Namba za simu au taarifa za mawasiliano za watoto.
  • Anwani au maeneo yanayoweza kumtambua mtoto.
  • Picha au taarifa binafsi za mtoto bila ruhusa inayofaa.
  • Maudhui yanayoweza kumdhuru au kumdhalilisha mtoto.

Lengo la sheria hii ni kuhakikisha kuwa watoto wanalindwa dhidi ya madhara, unyanyasaji au kufichuliwa taarifa zao binafsi.

Hatua Zitakazochukuliwa

Confession yenye taarifa zinazoweza kuhatarisha mtoto itazuiwa au kuondolewa mara moja.

10

Hairuhusiwi Kujifanya Mtu Mwingine

Kila mtumiaji anatakiwa kutumia jukwaa hili kwa uaminifu. Hairuhusiwi:

  • Kujifanya wewe ni mtu mwingine.
  • Kutumia jina au utambulisho wa mtu mwingine kwa lengo la kumchafua au kumdanganya.
  • Kutengeneza confession ya uongo kwa kutumia taarifa za mtu mwingine.
  • Kujifanya mwakilishi wa Siri za Chumbani au timu ya usimamizi bila ruhusa.

Sheria hii imewekwa ili kulinda watu dhidi ya udanganyifu, kashfa na matumizi mabaya ya utambulisho.

Hatua Zitakazochukuliwa

Mtumiaji anayekiuka sheria hii anaweza kuzuiwa kutumia huduma za Siri za Chumbani na maudhui yake yataondolewa.

11

Hairuhusiwi Kutuma Spam au Matangazo Yasiyoruhusiwa

Siri za Chumbani si sehemu ya kutangaza bidhaa, huduma au ujumbe wa kibiashara bila ruhusa. Hairuhusiwi:

  • Kutuma ujumbe uleule mara nyingi.
  • Kutangaza biashara binafsi ndani ya confession.
  • Kushiriki viungo vya matangazo yasiyoidhinishwa.
  • Kutumia jukwaa kupata wateja au kufikisha ujumbe wa kibiashara bila idhini.

Sheria hii inasaidia kuhakikisha kuwa jukwaa linabaki kuwa sehemu ya kushirikiana siri na uzoefu wa maisha, badala ya kujazwa na matangazo yasiyohusiana.

Hatua Zitakazochukuliwa

Spam na matangazo yasiyoruhusiwa yataondolewa na mtumiaji anaweza kuzuiwa kutumia huduma ya kutuma confession.

12

Hairuhusiwi Matumizi Mabaya ya Jukwaa

Siri za Chumbani imejengwa kwa ajili ya kusaidia watu kueleza hisia zao na kushiriki uzoefu wao kwa njia salama. Hairuhusiwi kutumia jukwaa hili kwa madhumuni mabaya kama:

  • Kujaribu kuvuruga mfumo wa jukwaa.
  • Kutuma ujumbe mwingi kwa lengo la kuharibu huduma.
  • Kutafuta mianya ya kuvunja usalama wa jukwaa.
  • Kutumia huduma kwa njia inayoweza kuwaathiri vibaya watumiaji wengine.
  • Kujaribu kukwepa sheria au mifumo ya ukaguzi iliyowekwa.

Kila mtumiaji anawajibika kutumia jukwaa hili kwa njia inayolinda jamii yote ya Siri za Chumbani.

Hatua Zitakazochukuliwa

Team ya Siri za Chumbani ina haki ya kuchukua hatua stahiki ikiwemo kuzuia matumizi ya huduma, kuondoa maudhui husika au kuchukua hatua nyingine kulingana na uzito wa ukiukwaji.

Wajibu wa Pamoja

Siri za Chumbani inaamini kuwa kila mtu anastahili nafasi ya kueleza yaliyomo moyoni mwake kwa uhuru na usalama. Hata hivyo, uhuru wa kutoa maoni unaambatana na wajibu wa kuheshimu faragha, utu na usalama wa wengine. Kwa kufuata sheria hizi, kila mtumiaji anachangia kujenga jukwaa bora, salama na lenye kuaminika kwa watu wote.

Sheria Zinaweza Kubadilika Muda Wowote

Mnyilinga Digital inahifadhi haki kamili ya kubadilisha, kurekebisha, kufuta au kuongeza kifungu chochote cha sheria hizi, muda na wakati wowote, bila taarifa ya awali au idhini ya mtumiaji. Toleo jipya linapochapishwa, linatumika mara moja kwa watumiaji wote. Ni wajibu wa kila mtumiaji kufuatilia na kujisomea sheria hizi mara kwa mara.